Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Tume) ni Taasisi ya Serikali inayojitegemea iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Sura ya 171. Jukumu kuu la Tume ni kufanya mapitio ya Sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa mapendekezo ya kuziboresha ili ziandane na mazingira ya wakati uliopo kwa maendeleo endelevu. Pia Tume ina jukumu la kutoa Elimu ya Sheria kwa Umma ili kujenga uelewa wa Sheria katika jamii.
Tume inatekeleza majukumu yake kwa namna mbili: kwanza, kwa kupokea maelekezo kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Sheria au Mwanasheria Mkuu wa Serikali . Pili, Tume kwa uamuzi wake yenyewe hufanya mapitio au tathmini ya Sheria sambamba na kumtaarifu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu mapitio au tathmini ya Sheria husika. Tume inapotekeleza majukumu yake kwa namna ya pili, inaweza kupokea maombi kutoka idara au taasisi ya Serikali au isiyo ya Serikali au kutoka kwa jamii.