Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro, amezitaka Wizara na Taasisi zinazohitaji Kurekebisha au kutunga sheria kuitumia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya utafiti kwa kuwa ndio Taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kisheria ya kufanya tafiti za marekebisho au maboresho ya Sheria. Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 24.03.2025 katika ukumbi wa Bunge wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Amesema kwamba zipo taasisi ambazo zimekuwa zikileta mapendekezo ya kutunga au kurekebisha sheria Bungeni bila kuzingatia takwa kufanya utafiti wa kina jambo ambalo huchangia sheria hizo kupoteza uhalisia ndani ya kipindi kifupi. “zipo wizara ambazo zimekuwa zileta sheria mbele ya kamati posipokufanyiwa utafiti wa kisheria, ndani ya Serikali, Mtafiti wa Sheria anayetambulika kwa mujibu wa Sheria za Nchi ni Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania " Alisema Mhe. Ndumbaro. Amesema kuwa, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ndio chombo maalumu kinachotambulika ki sheria kwa kufanya utafiti kuhusu sheria zote hapa nchini na sio vyuo vikuu kama wanavyofanya na baadhi ya Wizara na Taasisi mbalimbali na hatua hizo zimekuwa zikifanyika pengine kwa kutumia gharama kubwa na hatimaye Sheria zinazokusudiwa kukosa tija zinapotungwa Alisisitiza kwamba, ili kufanikisha mabadiliko bora ya Sheria, Wizara na Taasisi za Serikali zinazohitaji kuboresha au kubadilisha sheria, zinapaswa kuchukua hatua za kutumia Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya tafiti na mapitio ya Sheria badala ya kuamua zenyewe bila kuwa na msingi wa kisheria kama ilivyo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo inatekeleza majukumu hayo chini ya Sheria yake. Alikumbusha kwamba, kwa kutumia Tume, mchakato wa mapitio na mabadiliko ya sheria unaweza kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa, alisistiza Mhe Dkt. Ndumbaro .