Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WAZIRI DKT. DAMAS NDUMBARO AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA MKOANI KAGERA
15 Apr 2025
WAZIRI DKT. DAMAS ND...

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amezindua kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) mkoani Kagera. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Tarehe 14 Aprili 2025 katika uwanja wa Mashujaa mjini Bukoba, Waziri Ndumbaro amewataka wananchi kutumia fursa hiyo ya msaada wa kisheria iliyowafikia ili kujipatia elimu juu ya Sheria mbalimbali katika kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili. “Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema Binadamu wote ni sawa, usawa huo ndio tunakusudia kuuleta kupitia Kampeni hii na tukipata haki na kuleta usawa tutajenga amani na Nchi ikiwa na amani ndipo tutapata maendeleo” alisema Dkt. Ndumbaro Katika hatua hiyo Dkt. Ndumbaro pamoja na kuhimiza wananchi kujitokeza kupata msaada wa kisheria amewataka Mawakili na wadau wa sheria wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria kuhakikisha wanawasaidia wananchi wa Kagera katika kutatua changamoto zao za kisheria zinazowakabili. Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imetumia fursa hiyo kushiriki katika kampeni ili kutoa Elimu ya Sheria kwa Umma na Msaada wa Kisheria  kwa wananchi. Mkoa wa kagera ni wa 25 kufikiwa na kampeni hiyo inayolenga kusaidia wananchi wa hali za chini wasio na uwezo wa kuwalipa mawakili binafsi kushughulikia changamoto zao za kisheria.