Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma wafikia asilimia 64%. Akizungumza mapema leo tarehe 18/3/2025 baada ya kutembelea na kukagua muendelezo wa ujenzi wa Jengo hilo wakati wa kikao cha 12 cha Kamati ya Usimamizi wa Ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (DCS) Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Jengo hilo, Bw. Mohamed Mavura amempongeza Mkandarasi anaejenga Jengo hilo kampuni ya LI JUN DEVELOPMENT CONSTRUCTION CO. LTD kwa kasi nzuri ya ujenzi anayoionyesha katika ujenzi wa jengo hilo. Aidha Mavura amemtaka Mkandarasi huyo wa kampuni ya LI JUN DEVELOPMENT CONSTRUCTION CO. LTD kuwa pamoja na juhudi kubwa anayoionesha anapaswa kutopunguza kasi katika kuhakikisha Jengo hilo linakamilika kwa wakati na kwa mujibu wa Mkataba ili liweze kuanza matumizi ya kutoa huduma kama ilivyokusudiwa. “Nawasihi muendeleze kasi ya ujenzi na kwa kuzingatia ubora ili kukamilisha kwa wakati na yale yote tuliyokubaliana katika kikao hiki na vikao vingine vilivyopita tuhakikishe tunayatimiza” alisema Mavura akimueleza Mkandarasi mbele ya wajumbe wa kamati ya usimamizi wa ujenzi wa Jengo hilo. Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania unagharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania 24,680,651,572.45/=, unategemewa kukamilika baada ya miezi 24 ambapo ulianza kutekelezwa Mwezi Novemba mwaka 2023 na unategemewa kukamilika Mwezi Desemba 2025.