Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA YAKABIDHI TAARIFA MBILI (2) ZA UTAFITI NA MAPITIO YA SHERIA KWA WAZIRI DKT. DAMAS NDUMBARO.
24 Mar 2025
TUME YA KUREKEBISHA...

  Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekabidhi Taarifa mbili (2) za Utafiti na Mapitio ya Sheria zilizofanyika katika mwaka wa Fedha 2023/2024 na 2024/2025. Kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ili kuruhusu hatua zingine kuendelea juu ya sheria hizo. Taarifa hizo ni Taarifa ya Mapitio ya Sheria ya Takwimu, Sura ya 351; na Taarifa ya Utafiti kuhusu Mfumo wa Sheria zinazosimamia Vyama vya Ushirika, ambazo zimekabidhiwa tarehe 24 Machi 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Katiba na sheria Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. Akizungumza mara baada ya kupokea Ripoti hizo Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro licha ya kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania, alisema Tume hiyo ndiyo Taasisi kuu ya Utafiti wa Sheria nchini na ndiyo yenye mamlaka kisheria kufanya mapitio na kupendekeza maboresho ya sheria yenye tija na ya kudumu ili sheria hizo ziendane na wakati. Katika hatua hiyo Dkt. Ndumbaro alieleza wazi kuhusu utekelezaji wa 4R za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Tume inatekeleza kwa vitendo kwa kufanya tafiti na Mapitio ya kisheria akibainisha kufanya hivyo ni kutimiza jukumu hilo kwa usahihi kwa kufanya tafiti, mapitio na  tathmini  zinazolenga maendeleo ya nchi kulingana na mabdiliko ya kijamii na kiuchumi duniani. “Ninaamini kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa hizi yatakidhi  kiu na matarajio ya wananchi na wadau mbalimbali ili kuleta mabadiliko ya namna ya utendaji na utoaji huduma kwa wananchi wa  taasisi zetu nchini.” Awali alipozungumzia kuhusu maandalizi ya taarifa hizo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzani Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe, Winifrida Korosso alisema Mchakato wa uandaji wa taarifa hizo umehusisha hatua mbalimbali za kitafiti ikiwemo vikao vya majadiliano na wadau (Stakeholders Consultative Meetings), uchambuzi wa hoja za awali, mapitio ya makala , machapisho, nyaraka, sera, sheria za ndani na sheria za nchi nyingine. Aidha Tume imepitia  mikataba ya kimataifa na kikanda, na kueleza kuwa Wadau mbalimbali wameshiriki katika kila kazi ya Utafiti na Mapitio. Akieleza zaidi kuhusu taarifa ya Mapitio ya Sheria ya Takwimu , Mhe. Korosso alisema Tume imebaini kuwapo kwa changamoto za kisera, kisheria na kiutawala zinazochangia kukosekana kwa mazingira wezeshi ya uwasilishaji wa takwimu rasmi NBS ambayo  ndiyo taasisi inayoratibu Takwimu nchini na Msimamizi wa Kanzidata ya Taifa ya Takwimu rasmi nchini.  Kwa upande wa Taarifa Utafiti kuhusu Sheria zinazosimamia Vyama vya Ushirika zikibainika changamoto kadhaa zikiwamo Kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kusimamia mitaji, fedha, mali na madeni ya vyama vya ushirika nchini. “Aidha pamoja na changamoto hizo na zinginezo zilizoanishwa katika taarifa Tume imetoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo” alisema Mhe. Korosso kwa msisitizo. Kwa upande wake Bw. Gerge Mandepo ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alisema mpaka sasa Tume hiyo imeshawasilisha jumla ya Taarifa 11 za sheria mbali mbali katika kipindi cha 2023/2025 na kuahidi kuongeza bidii ya kuzipitia sheria nyingi zaidi ili kuleta mabadiliko yenye tija. “ ..tunashukuru kwa Wizara ya Katiba na Sheria kutuongezea bajeti ya 46% sasa, hii inatupa nguvu kuongeza kasi ya kuzifanyia marekebisho sheria nyingi zaidi kwa kufanya tafiti, mapitio na tathmini ili kuongeza tija katika sheria mbali mbali” alisema Mandepo.