Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA YAELEKEZWA KUFANYA UTAFITI JUU YA SHERIA YA ARDHI .
16 Apr 2025
TUME YA KUREKEBISHA...

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya Utafiti juu ya Sheria ya Ardhi kuhusu umilikishaji wa ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja (Double Allocation) ambalo ni tatizo sugu katika jamii.

Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo tarehe 15 Aprili, 2025 wakati akiendelea na ziara ya kikazi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa wananchi wa Wilaya za Misenyi na Karagwe mkoani Kagera.

Alisema kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imebaini kuwapo kwa migogoro mingi ya ardhi, mirathi, unyanyasaji wa kijinsia, ukatili na mengineyo huku akibainisha kuwa Migogoro ya ardhi ndio inayoongoza kwa wananchi wengi katika mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla.

Hatua hiyo imepelekea Waziri wa Katiba na Sheria kuielekezaTume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya utafiti juu ya Sheria ya Ardhi ili kupendekeza mabadiliko yatakayotatua changamoto za namna hiyo.

Natoa maelekezo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya Utafiti wa suala hili la Double allocation sasa hivi ni Jinai kupitia TAKUKURU nataka iwe Jinai sasa kupitia Sheria za Ardhi” alisema Dkt. Ndumbaro.

Aidha Dkt.Ndumbaro ameeleza kuwa kufanya Tafiti na kutoa mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria hiyo kutaipa nguvu zaidi ya kudhibiti vitendo hivyo kwakuwa wahusika watabanwa kwa Sheria za TAKUKURU na kupitia Sheria za Ardhi.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inashiriki katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria Mama Samia (Mama Samia Legal Aid) kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria na elimu ya sheria kuhusiana na maboresho ya Sheria kwa wananchi.