Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) Imetakiwa kufanya tafakuri katika falsafa Nne (4R) za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani ili kuwatambua, kuainisha na kufanya maridhiano na wadau wa sheria kwa lengo la kuelewa changamoto za kisheria na namna ya kuzitatua. Maelekezo hayo yametolewa tarehe 10/04/2025 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Tanga beach Resort iliyopo mkoani Tanga. Dkt. Ndumbaro amesema ni muhimu kufanya tafakuri ya falsafa ya nne ya Rebuilding kwa kuwa itasaidia kubaini umuhimu wa kuboresha sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambayo kwa sasa haijaweka bayana (clarity) baadhi ya mambo na kusababisha taasisi nyingine zisizokuwa za utafiti wa sheria kufanya maboresho ya sheria pasipo kushirikisha Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. “Nataka Tume ifanye tafakuri katika falsafa nne za Mama Samia Suluhu Hassani ambapo Falsafa ya nne ya Rebuilding itasaidia kubaini namna ya kufanya maboresho ya sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwakuwa sheria hiyo haijaweka bayana baadhi ya mambo. Hii inachangia taasisi nyingine kufanya mabadiliko ya sheria bila kuishirikisha Tume” Ndumbaro Aidha Dkt. Ndumbaro amesisitiza Tume hiyo kuhakikisha inaongeza ubora wa tafiti wanazozifanya kuwa za kitaalamu zaidi kwa kuwashirikisha wabobevu wa maeneo mbalimbali ya sheria hata kwa kuwaazima wataalamu kutoka taasisi nyingine ikiwemo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hata hivyo amewakumbusha watafiti wa Tume hiyo kuhakikisha wanazingatia maslahi mapana ya nchi , historia ya nchi na mambo mengine ya kijamii wakati wa utafiti wa sheria mbalimbali kwa kuwa si kila eneo linafikiwa na sheria. Mwisho